TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa zaidi kuhusu Mahujaji kutoka Tanzania waliofariki na kujeruhiwa huko Saudi Arabia.
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kupitia Ubalozi wake mjini
Riyadh, Saudi Arabia imepokea taarifa kuwa hadi kufikia tarehe 27
Septemba, 2015 watu waliopoteza maisha kufuatia tukio la mkanyagano
(stampede) wa Mahujaji waliokuwa wakielekea Jamarat kutupa vijiwe huko
Mina nje kidogo ya mji wa Makkah, lililotokea siku ya Alhamisi tarehe 24
Septemba, 2015 wameongezeka na kufikia 769 na majeruhi 934.
Aidha,
Wizara kupitia Ubalozi huo inaendelea kufuatilia hatma ya Mahujaji wa
Tanzania waliopotea katika tukio hilo la ajali ambapo hadi sasa Mahujaji
wa Tanzania wapatao 50 bado hawajaonekana. Vikundi wanavyotoka Mahujaji
hao na idadi yao ni kama ifuatavyo:-
1. Ahlu Daawa-Mahujaji 30;
2. Khidma Islamiya-Mahujaji 16; na
3. TCDO-Mahujaji 4
Vile
vile juhudi za Ubalozi kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na
viongozi wa vikundi vilivyopoteza Mahujaji wao zimefanikiwa kuutambua
mwili wa hujaji mmoja aliyefariki dunia anayejulikana kwa jina la Shafi
Khamis Ali kutoka kikundi cha Ahlu Daawa. Kutambuliwa kwa mwili wa
hujaji huyo kunafanya idadi ya Mahujaji wa Tanzania waliofariki dunia
katika ajali hiyo kufikia watano (5).
Pia,
Wizara kupitia Ubalozi wake imepokea taarifa ya kupatikana kwa hujaji
mwingine anayeitwa Nasra Abdullah akiwa hai naye kutoka kikundi hicho
cha Ahlu Daawa.
Kuhusu
majeruhi, taarifa kutoka Ubalozini zinaeleza kuwa, hujaji mmoja
aliyejulikana kwa jina la Mahjabin Taslim Khan alipata majeraha
yaliyopelekea kukatwa mguu na kwa sasa anaendelea kupata matibabu huku
hali yake ikiendelea vizuri.
Ubalozi
unaendelea na juhudi za kuwatafuta Mahujaji wengine wa Tanzania ambao
bado hawajaonekana kwa ajili ya kubaini wale waliofariki au majeruhi
wanaoendelea kupatiwa matibabu.
Mahujaji
wengine wa Tanzania wapo salama ambapo tarehe 26 Septemba, 2015
walimaliza ibada ya hija na tarehe 28 Septemba, 2015 wameanza safari ya
kurejea nyumbani.
Wizara inaendelea kuwaomba Wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Serikali ikiendelea kufuatilia.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
28 Septemba, 2015
No comments:
Post a Comment