Na Mwandishi wetu
Redds Miss Tanzania 2012 ambaye pia ni
Redds Miss Sinza, Brigitte Alfred amewataka warembo wanaowania taji la mwaka
huu la kituo cha Sinza kutomuangusha kwa kufauata nyayo zake katika
shindano lililopangwa kufanyika Juni 8 kwenye ukumbi wa Meeda Club.
Brigitte alisema hayo juzi
alipotembelea warembo wanaowania taji la mwaka huu katika kinyang’anyiro hicho
kilichodhaminiwa na bia ya Redds Origional, Dodoma Wine, Clouds Media Group,
Chilly Willy Energy Drink, Fredito Entertainment, CXC Africa, Saluti5.com na
Sufiani Mafoto blog.
Alisema kuwa warembo wa kituo
hicho wanakazi kubwa ya kushinda taji hilo na baadaye Miss Kinondoni na Miss
Tanzania kama yeye alivyofanya.
Alifafanua kuwa siri kubwa ya mafanikio
ni kujituma na kuwa na nidhamu ya hali ya juu kwani hata yeye alifundishwa na
matroni wa sasa, Mwajabu Juma na waandaaji ni wale wale.
“Sioni sababu ya kushindwa kufanya
vyema katika mashindano haya, Redds Miss Sinza ndiyo inatetea taji la Miss
Kinondoni na Miss Tanzania pia, hivyo macho ya wadau wote wa urembo yatakuwa
kwenu na ndicho kitongoji kinachofunga mashindano ya ngazi ya chini, mnatakiwa
kujituma na kuwafanya majaji kuwa na kazi ya ziada kumpata mshindi,” alisema
Brigitte.
Alisema kuwa wadau wa masuala ya urembo
wanaangalia Sinza mwaka huu itafanya nini baada ya mafanikio makubwa ya mwaka
jana. “Sisi tumejenga msingi mkubwa na kuleta heshima kwa wakazi wa
Sinza, Kinondoni na Tanzania kwa ujumla, nanyi mna jukumu hilo,” alisema.
Mratibu wa mashindano hayo, Majuto
Omary alisema kuwa maandalizi yamekwisha kamilika na kiingilio ni sh 10,000 kwa
viti vya kawaida na shs 20,000 kwa viti vya VIP. Alisema kuwa wanakamilisha
maandalizi ya burudani ya siku hiyo ambayo itakuwa ya aina yake.
No comments:
Post a Comment