SHIRIKISHO
la Muziki Tanzania (TMF) kwa kushirikiana na kamati ya kuratibu mazishi ya
marehemu Albert Mangwea limewaomba watanzania kushiriki katika kuchangia fedha
kwa ajili ya kuusafirisha mwili wa msanii huyo kutoka Afrika Kusini kuja
nyumbani Tanzania.
Wakizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, viongozi wa TMF na kamati
hiyo walisema kwa kuwa kuna gharama kubwa kama vile kusafirisha mwili kutoka Afrika ya
Kusini na kuusafirisha mpaka Morogoro,
usafiri, vyakula, viti, matangazo na malazi hivyo watanzania wachangie
kufanikisha hayo.
Msemaji wa
kamati hiyo Adam Juma alisema wanatambua
kwamba watanzania wanaukumbuka mchango wa marehemu jinsi alivyowahudumia kwa
kuwaburudisha hivyo, wanaomba watanzania kujitokeza kwa wingi na kuchangia.
“Tunaomba tushirikiane
sote kwa pamoja katika kipindi hiki kigumu ili kufanikisha yale tuliyopanga,
”alisema.
Alisema
mchango unaweza kuwasilishwa kupitia M pesa ya kaka wa marehemu Keneth Mangwea
0754967738 au Tigo Pesa 0717553905.
Juma alisema
wanampa pole mwanamuziki Mgaza Pembe M2P na kuomba maombi ya watanzania
kumwombea na kuendelea kumchangia mwanamuziki huyo ambaye alikuwa Afrika Kusini
na marehemu, ambaye mpaka sasa amelazwa katika hospitali ya St. Helen nchini
Afrika Kusini.
Kwa upande
wake Rais wa Shirikisho hilo Addo Mwasongwe amewaomba watanzania kutomtuhumu
msanii marehemu Mangwea kwenye mitandano
na badala yake wasubiri kwanza uchunguzi kutoka katika hospitali ya St,
Helen huku pia wakiendelea kumwombea.
Baadhi ya
wasanii waliokuwepo katika mkutano huo na waandishi wa habari, walizungumzia
jinsi walivyoguswa na msiba huyo na kusema hawatamsahau Albert Mangwea
alivyokuwa mkarimu na mtu wa watu kwani alikuwa ni rafiki wa kila mtu.
Wasanii hao
ni TID, Juma Mchopanga maarufu kama Jay Moe, Professa J, Noora, Mez B,
mtayarishaji wa muziki P fun Majani na wengine.
Mwili wa
Albet Mangwea utawasili Jumamosi jioni na kuhifadhiwa ambapo Jumapili kuanzia
saa mbili asubuhi katika viwanja vya Posta au Leaders au Biafra utaagwa na
wananchi na jioni kusafirishwa Morogoro Kihonda kwa ajili ya mazishi Juni 3.
No comments:
Post a Comment