Na
Mwandishi wetu
MREMBO wa
Tanzania, Brigitte Alfred ameanza ujenzi
wa bweni la wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (albino) katika wilaya ya
Shinyanga wanaoishi katika shule maalum ya Buhangija.
Tayari
mrembo huyo ameweka jiwe la msingi na kupandisha ukuta sambamba na kukabidhi
mabati 200 kwa ajili ya kujengea paa la bweni hilo la wavulana lenye uwezo wa
kulaza wanafunzi 50.
Makabidhiano
hayo yalifanywa na mrembo huyo kwa katika hafla fupi iliyohudhuriwa na mkuu wa
wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi, Afisa elimu wa Manispaa ya Shinyanga
Honoratha Ruhumbika na walimu wa shule hiyo wakiongozwa na mwalimu mkuu, Peter
Ajali.
Briggite
alisema kuwa ameamua kutimiza ahadi yake aliyoitoa mwezi Aprili mwaka huu
alipotembelea Shinyanga kwa kazi za jamii na kuona changamoto za watoto
wanaosoma katika shule hiyo.
Alisema
kuwa mpango huo upo katika mpango wa Miss Tanzania ujulikano kwa jina la Urembo
wenye malengo maalum (Beauty with Purpose) na yeye kuamua kufanya kwa vitendo.
“Ni
faraja kwangu kuona kuwa ninatimiza ahadi yangu, nawashukuru wote
walionisaidia ikiwa pamoja na familia yangu, na ninaomba wengine
wanisaidie kwani kuna changamoto nyingi katika ujenzi na kazi za jamii kwa
ujumla,” alisema Brigitte.
Alisema
kuwa amepania kuweka historia katika fani hiyo kwani anaamini ujenzi au jengo
hilo litakuwa kumbukumbu kubwa kwake tena kwa vizazi na vizazi.
Brigitte
pia aliwataka wanafunzi hao kutokata tamaa hata kwa wale wasiokuwa karibu na
familia zao na kwamba wamtegemee zaidi Mwenyezi Mungu kwa kuwa yeye ndiye mfariji
kwa wanyonge huku akiwahimiza kuzingatia zaidi elimu kwani ndiyo msingi wa
maisha yao.
“Nilipata
msukumo wa kuisaidia shule hii hususani katika ujenzi wa bweni hilo
kutokana na ujio wake wa mwezi Aprili mwaka huu shuleni hapo na kujionea adha
wanayopata watoto hao kutokana na msongamano mkubwa mabwenini,” alisema.
Mkuu wa
wilaya ya Shinyanga Annarose Nyamubi alimpongeza Brigitte kwa moyo huo wa
kujitolea na kuwataka warembo wengine kuiga mfano wake.
Nyamubi
alisema kuwa alichokifanya Brigitte ni jambo la kukumbukwa na ni msaada mkubwa
kwa jamii hasa kwa watu wenye ulemabu wa ngozi.
Mkuu huyo
wa wilaya aliwaomba wazazi wa watoto hao kuwa na tabia ya kuwatembelea watoto
wao mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kuwachuku wakati wa likizo.
Naye
mwalimu mkuu wa shule hiyo Peter Ajali alisema kuwa shule hiyo inakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo la msongamano mabweni kwani kuna jumla ya
watoto 247 huku mabweni yaliyopo yana uwezo wa kukaa watoto 148 tu.
No comments:
Post a Comment