TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday, 28 August 2013

Wanafunzi 1,800 kujiunga na chuo kikuu Liberia

Rais wa Liberia Sirleaf Johnson
   Rais wa Liberia, Ellen Sirleaf Johnson, amesema chuo kikuu kinachomilikiwa na serikali, kimekubali kuwasajili wanafunzi elfu moja mia nane ambao walifeli mtihani wa mwisho wa kitaifa wa shule ya upili.

Raos Sirleaf ameiambia BBC kuwa ameshauriana na maafisa wakuu wa chuo hicho kuhusiana na suala la wanafunzi wote waliofeli.

Takriban wanafunzi elfu ishirini na tano waliotahiniwa walianguka mtihani huo, huku maafisa wa elimu wakisema wengi wao hawana ufahamu wa lugha ya Kiingereza.

Liberia inaendelea kujinasua kufuatia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyomalizika zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Sirleaf alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka wa 2011, kwa juhudi zake za kumaliza mzozo wa kisiasa nchini humo, uliosababisha vifo vya zaidi ya watu laki mbili na kuharibu hali ya miundo mbinu ya taifa hilo la Afrika Magharibi.

Rais huyo ameiambia BBC kuwa, wasimamizi wa chuo hicho waliweka viwango vya kufuzu kuwa juu zaidi, na hivyo kuwafungia wanafunzi wengi nje.

Hata hivyo hakusema, kwa nini chuo hicho kilichoko mjini Monrovia, kimekubali kuwachukua wanafunzi elfu moja mia nane, baada ya mashauriano naye.

Akijibu wakosoaji wake ambao wanadai kuwa ameshindwa kuimarisha viwango vya elimu nchini humo tangu mwaka wa 2005, wakati alipochaguliwa kuwa rais, Bi. Sirleaf alisema'' Kwa hakika wao hawana msingi wowote, hakuna njia ya mkato kwa sasa''.

''Idadi ya wanafunzi waliojiunga na shule tangu nilipochaguliwa imeongezeka maradufu'' Alisema Bi. Sirleaf.

Chanzo.Bbc Swahili

No comments:

Post a Comment