TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Tuesday, 24 September 2013

Vikosi vya Kenya 'vimedhibiti' Westgate

 Na Bbc Swahili
 Hatimaye vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema vimelidhibiti jengo zima la Westgate mjini Nairobi, ikiwa ni zaidi ya siku tatu baada ya jengo hilo kuvamiwa na wanamgambo.

Milipuko ikifuatiwa na milio ya risasi imesikika kutoka ndani ya jengo hilo asubuhi ya leo huku duru zikisema kuwa vikosi vya usalama vinaelekea kukamilisha operesheni hiyo.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, magaidi sita waliokuwa wamesalia wameuawa huku wengine watatu wakiuawa hapo jana.

Serikali imesema zaidi ya watu 60 wameuawa na wengine zaidi ya 170 kujeruhiwa katika shambulio hilo ambalo Al shabaab imekiri kulitekeleza.

Wizara ya mambo ya ndani imesema wanajeshi wanaendelea kulisaka jengo zima la Westgate kutoka orofa moja hadi nyengine kuhakikisha kwamba hakuna mateka aliyesalia

Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje amesema kuwa wawili kati ya wanamgambo watatu waliofanya shambulii hilo ni raia wa Marekani pamoja na mwanamke muingereza.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni nchini Marekani, Amina Mohamed alisema kuwa wamarekani walikuwa kati ya umri wa miaka 18 na 19 ingawa wenye asili ya kisomali au kiarabu na waliishi mjini Minnesota. Mshukiwa mwingine alikuwa mwanamnke Muingereza ambaye inasemekana alikuwa amefanya vitendo vingi vya aina hii kwa niaba ya Al Shabaab.

Shirika la Red Cross limeambia BBC kuwa watu 63 wangali hawajulikani waliko.
Wanajeshi wa Kenya katika juhudi za kuokoa mateka na kukomboa jengo la Westgate

Haijulikani idadi ya wanamgambo waliokuwa ndani ya jengo hilo , lakini maafisa wa usalama wamesema kuwa wanamgambo watatu wameuawa.
Kundi la kigaidi la al-Shabab limekiri kutekeleza mauaji hayo, kulipiza kisasi hatua ya Kenya kujihusisha kijeshi nchini Somalia.

Operesheni hiyo iliendelea usiku kucha ingawa kwa mujibu wa waziri wa usalama wa Kenya, ilikuwa katika mkondo wake wa mwisho.

"magaidi hawa huenda wanakimbia na kujificha katika sehemu mbali mbali za jengo hilo lakini ghorofa zote za jengo hilo zimedhibitiwa na majeshi,'' alisema Ole Lenku

Aliongeza kuwa mateka wote walifanikiwa kuokolewa.
Jumatatu jioni moshi mkubwa ulionekana ukifuka kutoka kwenye jengo la Westgate ukiambatana na moto mkubwa. Moto huo unasemekana uliwashwa na wanamgambo hao ili kutatiza vikosi vya usalama katika juhudi zao za kutaka kukomboa jengo hilo.

No comments:

Post a Comment