By Isaac Mwangi,EANA
Arusha, Oktoba 12, 2013 (EANA)
– Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Juma Mwapachu
amependekeza kwamba mwaka 2014 utangazwe kuwa Mwaka wa Raia wa Afrika Mashariki
katika juhudi za kuzihamasisha nchi wananchama kuanza kujiona kuwa ni wana
Afrika mashariki.
Akizungumza katika siku
ya kwanza ya Mkutano wa Jukwaa la Katibu Mkuu wa EAC kwa sekta binafsi,asasi za
kiraia na wadau wengine mjini Nairobi,Kenya, Mwapachu alimshauri Katibu Mkuu wa
sasa wa EAC, Dk Richard Sezibera kutoa pendekezo hilo kwa baraza la mawaziri na
kisha katika kikao cha wakuu wa nchi kitakachofanyika mwezi ujao.
Mwapachu ambaye saa ni
Rais wa Chama cha Maendeleo ya Kimataifa alikuwa anawasilisha mada juu ya ‘’
Kuimarisha Mtangamano wa EAC:Jukumu la Raia.’’
Akichukua mfano kutoka
Umoja wa Ulaya (EU) alitoa wito wa kufanyia marekebisho mkataba wa EAC ili
kuweza kuanzisha Juhudi za kuwa na Uraia wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa EU ulifanyiwa
marekebisho na mkutano wa Lisbon,ambao ulianza kutumika rasmi Desemba 2009,kutoa
uraia kwa raia wa EU. Mwaka 2013, ulitangazwa na EU kuwa Mwaka wa Raia wa Umoja
wa Ulaya.
Tatizo kubwa
linaloikabili kanda ya EAC, Mwapachu alisema ni mtazamo wa washirika wakubwa
katika mtangamano wakiwemo viongozi wa siasa,vyombo vya habari na asasi za
kiraia kushughulikia mambo yanayohusu jumuiya kutoka katika misimamo ya
kitaifa.
‘’Katika hali kama hiyo
upo ukosefu mkubwa wa uelewa juu ya masuala ya kanda kinyume na masuala ya
kitaifa na hivyo kuleta matokeo hasa kwa EAC. Kutokana na hali kama hiyo
utahamasishaje fikra za uraia mpana katika mtangamano wa jumuiya nje ya semina,
mikutano na makongamano?,’’ aliuliza Mwapachu.
Mapema mkutano huo ulifunguliwa
rasmi na Katibu anayeshugulukia Wizara ya Masuala ya Afrika Mashariki, Biashara
na Utalii, Bi Phyllis Kandie, ambaye
alisisitiza umuhimu wa kuwa na mikutano kama hiyo mara kwa mara na wadau ili
kupata mawazo na maoni yao juu ya hatua mbalimbali za kuendeleza na kuboresha
mtangamano.
Katika hotuba yake
Katibu Mkuu wa EAC, Dk Sezibera alitoa changamoto kwa asasi za kiraia na sekta
binafsi kuimarisha ushirikiano mipakani na mitandao mbalimbali na mashirika ili
kulifikia lengo la kuleta umoja na mafanikio Afrika Mashariki.
IM/LC/NI
No comments:
Post a Comment