WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema anatamani
kuona Serikali za Mitaa hapa nchini zinasimamia maendeleo kuanzia ngazi ya
chini kwa kushirikiana na sekta binafsi ikiwa ni njia ya kuharakisha maendeleo
kwa wananchi.
Ametoa kauli hiyo huo leo mchana (Jumatatu, Novemba 25, 2013) wakati
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa
ushirikiano baina ya Mamlaka za Serikali za Mitaa za China na Tanzania ulioanza
leo jijini Dar es Salaam.
“Ni muhimu tukaanzisha ushirikiano huu kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa
kwa sababu usimamizi wake unakuwa karibu zaidi na wananchi kuliko ilivyo hivi
sasa”, alisema.
Kuhusu ujio wa magavana, mameya na
wafanyabiashara wapatao 71 kutoka majimbo manne ya Shandong, Liaoning, Shaanxi
na Jilin, Waziri Mkuu alisema ujio wao umekuja wakati muafaka kwani unasaidia
kujenga mahusiano ya karibu zaidi na wananchi kwenye ngazi ya chini kuliko
inavyokuwa kuna mahusiano kwenye ngazi ya Kitaifa peke yake.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda |
“Hawa waliokuja wanatoka majimbo
manne tu kati ya majimbo 31 ya nchi hiyo, tungependa kila mwaka tupate wajumbe
wa aina tofauti hadi tufikishe majimbo 15 au 20 hivi... tunataka ushirikiano
huu ukue zaidi uende hadi katika miji mikubwa ya Beijing ama Shanghai,”
aliongeza.
Katika hotuba yake kwa wajumbe wa
mkutano huo, Waziri Mkuu aliwataka watumie fursa hiyo kubadilishana uzoefu na
kufanikisha mahusiano ya kibishara si tu baina yao, bali hata katika ngazi ya
Halmashauri wanazotoka baadhi ya wajumbe.
Mapema akizungumza na washiriki wa
mkutano huo, Balozi wa China nchini Tanzania, Dk. Lu Youqing alisema biashara
kati aya China na Tanzania imeongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.47
ambalo ni ongezeko la asilimia 15.2 ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka
jana.
Alisema hadi kufikia Juni, 2013,
makampuni zaidi ya 500 kutoka China yalikuwa yamekwishasajiliwa hapa nchini
yakiwa na mtaji wa Dola za Marekani
bilioni 2.175 na kuifanya China iwe ni mwekezaji wa pili kwa ukubwa hapa nchini
Tanzania.
Naye Naibu Gavana wa Jimbo la
Shandong, Bw. Xia Geng ambaye pia ni kiongozi wa msafara huo, alisema Agosti,
2013 China ilileta madaktari 23 wa fani tofauti ili kusaidia kujenga kada ya
watalaam wa sekta ya afya hapa nchini.
Alisema maeneo makuu ambayo
wamelenga kuyazingatia katika ziara yao hii ni Kilimo; Nishati; Utunzaji wa
Mazingira na uchimbaji wa rasilmali za ardhini.
Alisema ifikapo mwaka 2014, wakati
Tanzania na China zinatarajiwa kuadhimisha miaka 50 ya urafiki baina yao,
angependa kuona maeneo hayo ya msingi yakiwa yamepewa kipaumbele katika
utekelezaji wake.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na
Waziri wa Nchi (OWM-TAMISEMI), Bibi Hawa Ghasia; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Asiyekuwa na Wizara Maalum), Prof. Mark Mwandosya, Wakuu wa mikoa 25, Makatibu
Tawala wa Mikoa 25, Wakuu wa Wilaya 50, Wakurugenzi wa Halmashauri 95 na
wafanyabiashara kadhaa.
No comments:
Post a Comment