Na Mwandishi wetu
Shirika la Madini la Taifa
[STAMICO] limeingia mkataba wa ubia na Kampuni ya TanzaniteOne Mining Limited
[Tanzanite One] kuhusu uchimbaji wa pamoja wa madini, ya Tanzanite katika
kitalu C, Mirerani.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini
Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa STAMICO Gray Mwakalukwa wakati akitoa
ufafanuzi kwa waandishi wa habari mara
baada ya hafla fupi ya kusaini mkataba huo.
Mwakalukwa alisema kuwa hatua
hiyo imefikiwa baada ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kutoa
leseni ambayo inawawezesha STAMICO kumiliki asilimia 50 na TanzaniaOne watabaki
na asilimia 50.
Alisema kuwa umiliki huo
unatokana na Serikali kusimamia utekelezaji wa Sera ya Madini ya mwaka 2009 na
Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambapo chini ya sharia hiyo, Kampuni za kigeni
haziruhusiwi kumiliki hisa zaidi ya asilimia 50 katika uchimbaaji wa vito.
Mwakalukwa aliongeza kuwa mkataba
huo umezingatia makubaliano ya awali yaliyotiwa saini mapema mwaka huu ambayo
yataka STAMICO na Tanzanite One kuwa na
gawio sawa la asilimia 50 kwa hamsini litakalotokana na faida.
Alitaja baadhi ya mambo
waliokubaliana ni pamoja na mitambo ya uchimbaji na uzalishaji itabaki kuwa ni
mali ya Tanzanite One itaendelea
kutumika na wabia wataifanyia matengenezo itakapoharibika.
Mwakalukwa alisema kuwa jambo
jingine waliokubaliana ni pamoja na kuanzisha kitengo maalum cha ufuatiliaji na
tathmini ya shughuli zote za mgodi kitakachoundwa kutoka kwa wajumbe wa kila
pande.
Naye Mwenyekiti wa Tanzanite One,
Balozi Ami Mpungwe alisema kuwa hatua ya
Kampuni yake kusaini mkataba huo ni
sehemu ya kutekeleza sera ya
uchimbaji wa madini nchini na ni hatua nzuri ya kuhakikisha
ulinzi na usalama madini ya Tanzanite.
No comments:
Post a Comment