KATIBU Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha la
vipaji vya sanaa na muziki lililoandaliwa na asasi ya ukuzaji vipaji
(Unscripted Concert for Africa-Tanzania, UCA-Tz).
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi Mtendaji wa asasi hiyo, Emmanuel Mushy alisema tamasha hilo
la pekee litakalofanyika Uwanja vya Biafra jijini Dar es Salaam
linatarajia kushirikisha vijana zaidi ya 500 kutoka maeneo anuai ya
jiji.
Akifafanua zaidi juu ya tamasha hilo, Mushy alisema
UCA-Tz ni program yenye dhumuni la kutoa nafasi kwa vijana wenye vipaji
vya muziki na sanaa ili vijana hao waweze kukua katika vipaji vyao.
“…Neno ‘unscripted’ linamaanisha kitu ambacho kipo lakini
hakijaandikwa, yaani kwa maana nyingine ni kitu kilichopo nyuma ya
pazia. UCA-Tz baada ya utafiti imebaini kuwa kuna vijana wengi ambao
wanajihusisha na muziki pamoja na sanaa lakini hawapati ile nafasi
(platform) ya kuendeleza vipaji vyao, hivyo ni kama vijana hawa wapo
nyuma ya pazia,” alisema Mushy.
Aliongeza kuwa UCA Tz kwa kutambua umuhimu wa vipaji
vya vijana vinavyopotea imeona umuhimu wa kutengeneza njia kwa vipaji
hivyo ili vitoke nyuma ya pazia kukua na hatimaye kujionesha kwa jamii.
Aidha alisema moja ya njia ambazo UCA-Tz inazifanya ni kuandaa matamasha
ya vipaji kwa kila mwaka kuwashirikisha vijana na kwa mara ya kwanza
inazindua Tamasha la vipaji nchini Tanzania, ambalo litashirikiza vijana
zaidi 500 kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
“…Tamasha hili la vipaji linatarajia kufanyika
kesho, Jumamosi ya tarehe 14th December pale Uwanja wa Kinondoni Biafra,
kuanzia saa 7 mchana hadi saa 12 za jioni. Katika tamasha hilo vijana
wenye vipaji vya kuimba, ku-rap, kucheza, kuchora na ubunifu (ku-design)
watawasilisha kazi zao kwa umati utakao jitokeza na vijana wenzao,”
alisema Mushy.
Alisema ili kuleta radha na hamasa zaidi asasi hiyo
imealika wawakilishi vijana kutoka nchi mbalimbali za Africa kama Kenya,
Uganda na Ghana ambao nao watashiriki. “…Kutakua na outside
performances kutoka kwa wasanii mbalimbali ambao wameshapiga hatua
kwenye tasnia za muziki na sanaa nao watashiriki kwa pamoja.
Naye Mwakilishi kutoka kampuni ya Zantel, Divine
Mosi ambao ni moja wa makampuni yaliofanikisha tamasha hilo, akizungumza
alisema kampuni yao itaendelea kuunga mkono shughuli anuai za
kuwawezesha vijana ikiwa ni sehemu ya kurudisha mchango wa wateja wao
wanaotumia mtandao wao.
Kampuni nyingine zilizounga mkono kiushirikiano
kufanikisha tamasha hilo ni pamoja na kampuni ya
Coca Cola, Maezeki, Arise Media, LGBY Media na mtandao wa kijamii wa
habari-Thehabari.com (www.thehabari.com) na mitandao mingine ya kijamii nchini.
No comments:
Post a Comment