Vigogo wa ligi kuu ya Uhispania ambao wamekuwa wakisuasua katika mechi za la liga Real Madrid, wamethibitisha udedea wao katika ligi ya mabingwa bara Uropa baada ya kuiadhibu vikali Borussia
Dortmund ya Ujerumani katika mkono wa kwanza wa robo fainali ya mchuano huo iliyochezwa Santiago Bernabeu.
Real iliilaza Borussia Dortmund mabao matatu kwa nunge .
Real ilidhihirisha nia yao mapema Gareth Bale alipofuma bao la kwanza kunako dakika ya tatu ya mechi hiyo.
Isco alitikisa wavu na bao la pili katika dakika ya 27, huku bao la tatu likifungwa naye Cristiano Ronaldo dakika ya 57 kipindi cha pili.
Bao hilo la mchezaji bora msimu wa 2013 lilimsaidia Ronaldo kusawazisha rekodi ya idadi kubwa ya mabao kuwahi kufungwa kwa msimu mmoja wa dimba hilo la mabingwa barani Uropa.
Bao la Ronaldo lilikuwa la 14 katika mechi nane za ligi ya mabingwa , sawia na rekodi iliyowekwa na Lionel Messi katika mwaka wa 2011-2012.
Kwa upande wao Dortmund ambao walishindwa katika fainali mwaka uliopita na Bayern Munich watajilaumu wenyewe kwa kutotumia vyema fursa 12 walizopata kushambulia lango la Real.
Hata hivyo vijana hao wa Jurgen Klopp walidhihirisha wazi bila nyota wao Robert Lewandowski safu yao ya ushambulizi ni butu.
Wajerumani hao wanajuma moja tu kusahihisha makosa walioyafanya jana kabla ya mechi ya marudio ambayo imeratibiwa kuchezwa tarehe 8 Aprili huko ujerumani.
Source:Bbc Swahili
No comments:
Post a Comment